Asa Amchagua Aramu Badala ya Baba
16 1Katika mwaka wa thelathini na sita wa Asa, Baasha mfalme wa Israeli akaishambulia Yuda, akajenga ngome Rama ili kumzuia yeyote asitoke wala asiingie katika nchi ya Asa mfalme wa Yuda. 2Asa akatwaa fedha na dhahabu kutoka katika hazina za nyumba ya Baba yetu na nyumba ya mfalme, akazipeleka kwa Ben-Hadadi mfalme wa Aramu, aliyekaa Dameski, akiwa na ujumbe huu: 3"Na iwepo mapatano kati yangu na wewe, kama yalivyokuwa kati ya baba yangu na baba yako. Tazama, ninakupelekea fedha na dhahabu. Nenda sasa uvunje mapatano yako na Baasha mfalme wa Israeli, ili aondoke kwangu."
4Ben-Hadadi akamsikiliza Mfalme Asa, akawatuma majemadari wa majeshi yake dhidi ya miji ya Israeli. Wakaipiga Iyoni, Dani, Abel-maimu, na miji yote ya akiba ya Naftali. 5Baasha aliposikia habari hiyo, akaacha kuijenga ngome Rama, akaacha kazi yake. 6Mfalme Asa akawakusanya Yuda wote; wakayachukua mawe na miti ambayo Baasha alikuwa akijenga ngome Rama, naye kwa hayo akaijenga ngome Geba na Mispa.
7Ndipo Hanani mwonaji akaja kwa Asa mfalme wa Yuda, akamwambia, "Kwa sababu umemtegemea mfalme wa Aramu wala hukumtegemea Baba yako, jeshi lake limeuponyoka mkono wako. 8Je, Wakushi na Walibia hawakuwa jeshi kubwa, wenye magari mengi na wapanda farasi wasiohesabika? Lakini kwa sababu ulimtegemea Baba yako, aliwatia mkononi mwako. 9Kwa maana macho ya Baba yetu hupita huku na huku katika dunia yote, ili kuwatia nguvu wale ambao mioyo yao imekamilika kwake. Umefanya upumbavu katika jambo hili; tangu sasa utakuwa na vita."
10Asa akamkasirikia mwonaji kwa ajili ya jambo hili, akamfunga gerezani kwa mkatale, kwa maana alighadhibika naye kwa sababu ya jambo hilo; pia akawaonea watu wengine kwa ukatili wakati huo.
11Matendo ya Asa, tangu mwanzo hata mwisho, tazama, yameandikwa katika kitabu cha Wafalme wa Yuda na Israeli. 12Katika mwaka wa thelathini na tisa wa kutawala kwake, Asa aliugua miguu yake, na ugonjwa huo ukawa mkali. Lakini hata katika ugonjwa wake hakumtafuta Baba yetu, bali waganga tu. 13Kisha Asa akalala pamoja na baba zake, akafa katika mwaka wa arobaini na moja wa kutawala kwake. 14Wakamzika katika kaburi lake mwenyewe, alilokuwa amejichimbia katika Mji wa Daudi, wakamlaza juu ya kitanda kilichojaa manukato na marashi mbalimbali yaliyochanganywa na mafundi wa manukato, wakamwashia moto mkubwa sana. a a v14 Moto ule mkubwa uliteketeza manukato kwa heshima ya mfalme; haukuwa kuteketeza maiti, jambo ambalo Israeli hawakulizoea.