Mfalme Aliyemtafuta Baba
26 1Kisha watu wote wa Yuda wakamfanya Uzia, mwenye umri wa miaka kumi na sita, kuwa mfalme mahali pa baba yake Amazia. 2Yeye akaijenga tena Elothi na kuirudisha kwa Yuda baada ya mfalme kupumzika pamoja na baba zake. 3Uzia alikuwa na umri wa miaka kumi na sita alipoanza kutawala, naye akatawala miaka hamsini na miwili huko Yerusalemu. Jina la mama yake aliitwa Yekolia wa Yerusalemu. 4Naye akafanya yaliyo mema machoni pa Baba yetu, sawasawa na yote aliyoyafanya baba yake Amazia. 5Akajitoa kumtafuta Baba yetu katika siku za Zekaria, aliyemfundisha kumcha Baba yetu; na alipokuwa akimtafuta Baba yetu, akafanikiwa.
6Akatoka na kupigana na Wafilisti, akazibomoa kuta za Gathi, na za Yabne, na za Ashdodi. Naye akajenga miji karibu na Ashdodi na kati ya Wafilisti. 7Baba yetu akamsaidia dhidi ya Wafilisti, na dhidi ya Waarabu waliokaa Gur-baali, na Wameuni. 8Waamoni wakamlipa Uzia ushuru, na sifa zake zikaenea hata mpaka wa Misri, kwa maana alikuwa amekuwa hodari sana. 9Uzia akajenga minara katika Yerusalemu penye Lango la Pembeni, na penye Lango la Bonde, na penye Pembe, akaiimarisha. a a v9 Pembe ilikuwa sehemu maalum iliyojitokeza ya ukuta wa mji wa Yerusalemu, tofauti na yale malango yaliyotajwa kwa majina. 10Akajenga minara jangwani, na kuchimba mabirika mengi ya maji, kwa maana alikuwa na makundi mengi ya wanyama katika nchi tambarare na uwanda. Tena aliwaweka wakulima na watunza mizabibu katika milima na katika mashamba yenye rutuba, kwa maana aliupenda udongo. 11Uzia alikuwa na jeshi la askari waliozoezwa, waliokwenda vitani kwa vikosi, kama walivyohesabiwa na Yeieli mwandishi na Maaseya msimamizi, chini ya Hanania, mmoja wa maakida wa mfalme. 12Jumla ya idadi ya viongozi wa jamaa waliowaongoza mashujaa hodari ilikuwa 2,600. 13Chini ya uongozi wao kulikuwa na jeshi la watu 307,500, waliozoezwa kupigana vita kwa nguvu nyingi, ili kumsaidia mfalme dhidi ya adui zake. 14Uzia akalipatia jeshi lote ngao, na mikuki, na chapeo, na dirii, na pinde, na mawe ya kombeo. 15Katika Yerusalemu akatengeneza vyombo vilivyobuniwa na watu wenye ustadi, vilivyowekwa juu ya minara na juu ya pembe, ili kurusha mishale na kutupa mawe makubwa. Na sifa zake zikaenea mbali sana, kwa maana alisaidiwa kwa ajabu hata akawa hodari.
Kiburi cha Uzia na Anguko Lake
16Lakini alipokuwa hodari, moyo wake ukajaa kiburi, hata akaangamia. Akawa si mwaminifu kwa Baba yetu, akaingia katika hekalu la Baba yetu ili kufukiza uvumba juu ya madhabahu ya kufukizia uvumba. 17Azaria kuhani akaingia nyuma yake, pamoja na makuhani themanini wa Baba yetu, watu hodari. 18Wakampinga mfalme Uzia, wakamwambia, "Si kazi yako, Uzia, kumfukizia Baba yetu uvumba, bali ni kazi ya makuhani, wana wa Haruni, waliowekwa wakfu ili kufukiza uvumba. Toka mahali patakatifu; kwa maana umekosa uaminifu, wala jambo hili halitakuletea heshima kutoka kwa Baba yetu."
19Ndipo Uzia akaghadhibika. Naye alikuwa na chetezo mkononi mwake ili kufukiza uvumba; na alipowaghadhibikia makuhani, ukoma ukatokea katika kipaji cha uso wake, hapo mbele ya makuhani katika nyumba ya Baba yetu, kando ya madhabahu ya kufukizia uvumba. 20Naye Azaria kuhani mkuu na makuhani wote walipomtazama, wakaona ukoma katika kipaji cha uso wake, wakamtoa haraka; naye mwenyewe akafanya haraka kutoka, kwa sababu Baba yetu alikuwa amempiga. 21Mfalme Uzia akawa na ukoma hata siku ya kufa kwake. Akakaa katika nyumba ya peke yake, hali akiwa na ukoma, akiwa ametengwa na nyumba ya Baba yetu. Naye Yothamu mwanawe akasimamia nyumba ya mfalme, akiwaamua watu wa nchi.
22Na mambo mengine ya Uzia, ya kwanza na ya mwisho, aliyaandika nabii Isaya mwana wa Amozi. 23Basi Uzia akapumzika pamoja na baba zake, wakamzika karibu na baba zake katika shamba la maziko lililokuwa la wafalme, kwa maana walisema, "Alikuwa na ukoma." Naye Yothamu mwanawe akatawala mahali pake.