Je, Kuna Tumaini kwa Mwanadamu?
14 1"Mwanadamu, aliyezaliwa na mwanamke, ana siku chache na amejaa taabu. 2Huchipuka kama ua kisha hunyauka; hukimbia kama kivuli wala hasidumu. 3Je, wewe humkazia macho mtu kama huyo? Nawe wanileta hukumuni mbele yako? 4Ni nani awezaye kutoa kitu safi kutoka katika kichafu? Hakuna hata mmoja. 5Kwa kuwa siku zake zimewekwa, hesabu ya miezi yake iko kwako, nawe umeweka mipaka asiyoweza kuivuka, 6geuza macho yako mbali naye, apate kupumzika, hata atakapomaliza siku yake kama mtu wa kuajiriwa.
7"Kwa maana lipo tumaini kwa mti: ukikatwa, utachipuka tena, na machipukizi yake hayatakoma. 8Ijapokuwa mzizi wake unazeeka ardhini na kisiki chake hufa mavumbini, 9kwa harufu ya maji utachipua na kutoa matawi kama mmea mpya. 10Lakini mwanadamu hufa na kulazwa chini; mtu hukata roho, naye yuko wapi? 11Kama maji yatowekavyo katika ziwa, na mto uishavyo na kukauka, 12vivyo hivyo mwanadamu hujilaza wala hainuki; hata mbingu zitakapokoma, hataamka wala kuamshwa katika usingizi wake.
13"Laiti ungenificha kaburini, ukanisitiri hata hasira yako itakapopita, ukaniwekea wakati uliopangwa, kisha ukanikumbuka! 14Kama mwanadamu akifa, je, atakuwa hai tena? Siku zote za utumishi wangu wa taabu ningengoja, hata upya wangu utakapokuja. 15Wewe ungeita, nami ningekujibu; ungeitamani kazi ya mikono yako. 16Kwa maana hapo ungehesabu hatua zangu; usingeweka macho juu ya dhambi yangu. 17Uasi wangu ungetiwa muhuri katika mfuko, nawe ungeifunika dhambi yangu.
18"Lakini kama mlima uangukavyo na kubomoka, na mwamba uondolewavyo mahali pake, 19kama maji yachakazavyo mawe na mafuriko yake yasombavyo udongo wa nchi, vivyo hivyo wewe waliangamiza tumaini la mwanadamu. 20Wewe humshinda nguvu milele, naye hupita zake; wewe waharibu uso wake na kumfukuza. 21Wanawe wapata heshima, wala yeye hajui; hushushwa chini, wala yeye hatambui. 22Yeye huhisi tu maumivu ya mwili wake mwenyewe, naye huomboleza kwa ajili yake mwenyewe tu."