Roho Yangu Imevunjika
17 1"Roho yangu imevunjika, siku zangu zimezimwa, kaburi liko tayari kwa ajili yangu. 2Hakika wenye dhihaka wamenizunguka, na macho yangu hayawezi kuachana na maudhi yao.
3"Weka rehani kwa ajili yangu kwako mwenyewe; ni nani mwingine atakayetoa neno lake kuwa mdhamini wangu? 4Kwa maana umezifunga akili zao zisipate ufahamu; kwa hiyo hutawaacha wapate ushindi. 5Yeye awashutumuye rafiki zake kwa faida yake mwenyewe—macho ya watoto wake yatazimia.
6"Amenifanya kuwa kitu cha kunenwa katika mataifa, mtu ambaye watu humtemea mate usoni. 7Jicho langu limefifia kwa huzuni, na viungo vyangu vyote ni kama kivuli. 8Wanyofu wanashangaa kwa jambo hili, na asiye na hatia hukasirika juu ya asiyemcha Mungu. 9Lakini mwenye haki hushikilia njia yake, na yeye aliye na mikono safi huzidi kuwa na nguvu zaidi na zaidi.
10"Lakini rudini, nyote, njoni sasa—sipati hata mtu mmoja mwenye hekima miongoni mwenu. 11Siku zangu zimepita, mipango yangu imekatika, na pamoja nayo tamaa za moyo wangu. 12Wao hugeuza usiku kuwa mchana; 'nuru,' wasema, 'iko karibu'—mbele ya giza. 13Kama nikitumaini kaburi kuwa nyumba yangu, kama nikitandika kitanda changu gizani, 14kama nikiliambia shimo, 'Wewe ndiwe baba yangu,' na funza, 'Mama yangu' na 'Dada yangu,' 15basi liko wapi tumaini langu? Ni nani awezaye kuona tumaini lolote kwangu? 16Je, litashuka hadi malango ya kaburi? Je, tutashuka pamoja mavumbini?"