Sofari Ajibu Tena
20 1Ndipo Sofari, Mnaamathi, akajibu: 2"Ndiyo sababu mawazo yangu yenye machafuko yananilazimu kujibu, kwa sababu ya msukosuko ulio ndani yangu. 3Nasikia karipio linalonivunjia heshima, na kutokana na ufahamu wangu roho hunichochea kujibu. 4Hakika wewe wajua jinsi ilivyokuwa tangu zamani za kale, tangu mwanadamu alipowekwa juu ya nchi: 5ushindi wa waovu ni wa muda mfupi, na furaha ya wasiomcha Mungu hudumu kitambo kimoja tu. 6Ijapokuwa kiburi chake hufika mbinguni, na kichwa chake hugusa mawingu, 7ataangamia milele, kama mavi yake mwenyewe; wale waliomwona watauliza, 'Yuko wapi?' 8Atatoweka kama ndoto, wala hatapatikana tena, akifukuzwa kama maono ya usiku. 9Jicho lililomwona halitamwona tena; wala mahali pake hapatamtazama tena. 10Watoto wake watawaomba maskini; na mikono yake mwenyewe itairudisha mali yake. 11Nguvu za ujana zijazazo mifupa yake zitalala pamoja naye mavumbini. 12Ijapokuwa uovu ni mtamu kinywani mwake, naye huuficha chini ya ulimi wake, 13ijapokuwa hataki kuuachilia, bali huushika kinywani mwake, 14lakini chakula chake huchacha tumboni mwake; huwa sumu ya fira ndani yake. 15Amezimeza mali, lakini atazitapika; Mungu atazitoa tumboni mwake. 16Atanyonya sumu ya fira; ncha ya nyoka itamwua. 17Hatayaona kamwe vijito, mito itiririkayo asali na maziwa mgando. 18Ni lazima airudishe tunda la taabu yake bila kulimeza; hatafurahia faida ya biashara yake. 19Kwa maana aliwaonea na kuwaacha maskini; ameinyakua nyumba asiyoijenga. 20Kwa sababu tumbo lake halikujua amani, hatapona pamoja na vitu alivyovitamani. 21Hakuna kilichosalia ambacho angekula; kwa hiyo ufanisi wake hautadumu. 22Katika wingi wa utajiri wake, dhiki itamfikia; uzito wote wa taabu utamjilia. 23Atakapokuwa ameshiba tumbo lake, Mungu atamfyatulia hasira yake iwakayo, na kuinyeshea juu yake iwe chakula chake. 24Ijapokuwa hukimbia silaha ya chuma, mshale wa shaba utamchoma. 25Auchomoa, nao hutoka mwilini mwake; ncha ing'aayo hutoka kwenye nyongo yake. Vitisho humwangukia. 26Giza totoro linawavizia hazina zake; moto usiowashwa na mtu utamteketeza na kula kila kilichosalia hemani mwake. 27Mbingu zitaidhihirisha hatia yake, na nchi itainuka juu yake. 28Utajiri wote wa nyumba yake utachukuliwa, ukafagiliwa mbali katika siku ya ghadhabu ya Mungu. 29Hii ndiyo sehemu ya mtu mwovu itokayo kwa Mungu, urithi aliowekewa na Mungu."