Kile Ambacho Mchimbaji Hawezi Kukichimbua
28 1"Hakika kuna machimbo ya fedha, na mahali ambapo dhahabu husafishwa. 2Chuma hutolewa katika mavumbi, na shaba huyeyushwa kutoka jiwe. 3Mwanadamu huweka mpaka kwa giza; hutafuta hadi mwisho kabisa madini yaliyo katika utusitusi na kivuli kizito. 4Huchimba shimo refu mbali na wanapoishi watu, mahali ambapo hakuna mguu uliowahi kukanyaga; huko wao huning'inia na kuyumbayumba, mbali na mtu yeyote. 5Nchi—kutoka kwake hutoka chakula, lakini chini yake hupinduliwa kama kwa moto. 6Mawe yake yana yakuti samawi, na mavumbi yake yana dhahabu. 7Ni njia ambayo hakuna ndege mwindaji aijuaye, ambayo jicho la kipanga halijawahi kuiona. 8Wanyama wenye kiburi hawajaikanyaga, wala simba hajapita juu yake akiwinda. 9Mwanadamu huweka mkono wake kwenye jiwe gumu na kuzipindua milima kwenye mizizi yake. 10Huchonga mifereji katika miamba, na jicho lake huona kila kitu cha thamani. 11Huyazuia maji yatiririkayo, na kuvitoa vitu vilivyofichwa nuruni.
12"Lakini hekima—yaweza kupatikana wapi? Na mahali pa ufahamu pako wapi? 13Mwanadamu haijui thamani yake, wala haipatikani katika nchi ya walio hai. 14Vilindi husema, 'Haiko ndani yangu,' na bahari husema, 'Haiko kwangu.' 15Haiwezi kununuliwa kwa dhahabu iliyo bora, wala bei yake haiwezi kupimwa kwa fedha. 16Haiwezi kuthaminiwa kwa dhahabu ya Ofiri, kwa akiki ya thamani au yakuti samawi. 17Dhahabu na kioo haviwezi kulingana nayo, wala haiwezi kubadilishwa kwa vyombo vya dhahabu safi. 18Marijani na kioo havistahili kutajwa; bei ya hekima huzidi lulu. 19Yakuti manjano ya Kushi haiwezi kulingana nayo, wala haiwezi kuthaminiwa kwa dhahabu safi.
20"Basi, hekima hutoka wapi? Na mahali pa ufahamu pako wapi? 21Imefichwa mbali na macho ya vyote vilivyo hai, imesitirika hata kwa ndege wa angani. 22Uharibifu na Mauti husema, 'Kwa masikio yetu tumesikia uvumi wake.'
23"Mungu anaifahamu njia yake, naye anapajua mahali pake. 24Kwa maana yeye huangalia hadi miisho ya dunia na kuona kila kitu kilicho chini ya mbingu. 25Alipoupa upepo uzito wake na kuyapima maji, 26alipoiwekea mvua amri na njia kwa radi ya ngurumo, 27ndipo alipoiona hekima na kuitangaza; aliithibitisha na kuichunguza.
28Naye akawaambia wanadamu, 'Kumcha Mungu—hiyo ndiyo hekima, na kujiepusha na uovu ndio ufahamu.'"