Bildadi Mshuhi Ajibu
8 1Ndipo Bildadi Mshuhi akajibu: 2"Hata lini utaendelea kunena mambo kama haya? Maneno ya kinywa chako si kitu ila upepo wa kishindo. 3Je, Mungu hupotosha hukumu? Je, Mwenyezi hupotosha haki? 4Kama watoto wako wamemtenda dhambi, aliwatia mkononi mwa matokeo ya uasi wao. 5Lakini kama utamtafuta Mungu kwa bidii na kumsihi Mwenyezi ili apate kukuhurumia, 6kama wewe u safi na mnyofu, bila shaka sasa atajiamsha kwa ajili yako na kukurudisha mahali pako pa haki. 7Ingawa mwanzo wako ulikuwa mdogo, miaka yako ya baadaye itasitawi kupita kiasi. 8Waulize vizazi vilivyopita zamani, na uyafikirie yale ambayo baba zao waliyachunguza. 9Kwa maana sisi tulizaliwa jana tu, wala hatujui neno; siku zetu duniani si kitu ila kivuli. 10Je, hawatakufundisha na kukuambia, na kutoa maneno yatokayo katika ufahamu wao? 11Je, mafunjo yaweza kukua marefu pasipo pahali penye matope? Je, manyasi yaweza kusitawi bila maji? 12Ingali mabichi bila kukatwa, hunyauka upesi kuliko majani yote. 13Ndiyo mwisho wa wote wamsahauo Mungu; ndivyo litakavyoangamia tumaini la asiyemcha Mungu. 14Uthabiti wake ni dhaifu, na matumaini yake ni utando wa buibui. 15Huitegemea nyumba yake, lakini haisimami; hushikamana nayo, lakini haidumu. 16Yeye ni kama mmea unyweshwao maji vizuri kwenye jua, ukieneza machipukizi yake bustanini. 17Mizizi yake hujizungusha juu ya chungu ya mawe na kutafuta mahali pa kushikilia kati ya miamba. 18Lakini atakapong'olewa mahali pake, mahali pale humkana, pakisema, 'Sikupata kukuona kamwe.' 19Ndiyo furaha ya njia yake—na kutoka udongoni wengine huchipuka mahali pake. 20Mungu hatamkataa mtu asiye na hatia, wala hatawapa mkono watendao maovu. 21Bado atakijaza kinywa chako kicheko, na midomo yako vigelegele vya furaha. 22Wale wakuchukiao watavikwa aibu, na hema ya waovu haitakuwapo tena."