Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.
Mara nne Daudi auliza hata lini — hata lini kusahaulika, hata lini kufichwa uso, hata lini kuchukua huzuni, hata lini adui kuwa juu yake. Hakuna kinachobadilika katika hali yake. Hata hivyo zaburi yageuka kwa upendo wa Baba yake, na yamalizika kwa kuimba juu ya wema aliokwisha pokea.
13 1Hata lini, Baba yangu, utanisahau? Hata milele? Hata lini utanificha uso wako?
2Hata lini nitashindana na mawazo yangu na kubeba huzuni moyoni mwangu mchana kutwa? Hata lini adui yangu atanishinda? 3Nitazame unijibu, Baba yangu; uyatie nuru macho yangu, nisije nikalala usingizi wa mauti.
4Adui yangu atasema, "Nimemshinda," na watesi wangu watafurahi nianguapo. 5Bali mimi nimeutumaini upendo wako thabiti; moyo wangu utafurahi katika wokovu wako. 6Nitamwimbia Baba yangu, kwa kuwa amenitendea mema sana.