Zaburi ya Daudi, ya kukumbusha.
Akiwa mgonjwa, majeraha yake yakitunga usaha, akiachwa na rafiki huku maadui wakipanga njama, Daudi anafuatilia hali yake hadi kwenye dhambi yake mwenyewe wala hataki kujibizana na washtaki wake. Anakaa kimya kama kiziwi na kumngoja Baba yake, yeye peke yake anayetazamia atajibu.
38 1Ee Baba wangu, usinikemee katika hasira yako, wala usiniadhibu katika ghadhabu yako. 2Kwa maana mishale yako imenizama ndani sana, na mkono wako umenishukia kwa nguvu. 3Hakuna afya mwilini mwangu kwa sababu ya hasira yako; hakuna uzima katika mifupa yangu kwa sababu ya dhambi yangu.
4Kwa maana maovu yangu yamepanda juu ya kichwa changu; kama mzigo mzito, ni mzito kunizidi. 5Vidonda vyangu vinanuka na kutunga usaha kwa sababu ya upumbavu wangu. 6Nimeinama na kusujudu chini sana; mchana kutwa naenda nikiomboleza. 7Kwa maana viuno vyangu vimejaa moto, wala hakuna uzima katika mwili wangu.
8Nimekufa ganzi na kupondwa kabisa; naugua kwa sababu ya machafuko ya moyo wangu. 9Ee Baba wangu Mwenye Enzi, shauku yangu yote iko mbele zako, wala kuugua kwangu hakukufichwa kwako. 10Moyo wangu unadunda, nguvu zangu zinaniishia ; hata nuru ya macho yangu imeniondoka. 11Rafiki zangu na wenzangu wanajitenga na mateso yangu, na jamaa zangu wa karibu wanasimama mbali.
12Wale wanaoutafuta uhai wangu wanategesha mitego yao; wale wanaonitakia mabaya wananena maangamizi na kupanga hila mchana kutwa. 13Lakini mimi ni kama kiziwi asiyesikia, kama bubu asiyeweza kusema wala hafumbui kinywa chake. 14Nimekuwa kama mtu asiyesikia, ambaye hana jibu kinywani mwake. 15Lakini nakungoja wewe, Baba wangu; ni wewe utakayejibu, Ee Baba wangu Mwenye Enzi.
16Kwa maana nilisema, "Wasije kamwe wakanifurahia mimi—wale wanaojigamba juu yangu mguu wangu unapoteleza." 17Kwa maana niko tayari kuanguka, na maumivu yangu yako mbele yangu daima. 18Naungama uovu wangu; nasumbuka kwa sababu ya dhambi yangu. 19Lakini adui zangu wana nguvu na wamejaa uhai, na wengi ni wale wanaonichukia bila sababu.
20Wale wanaonilipa mabaya kwa mema wananishtaki kwa sababu nafuatia lililo jema. 21Usiniache, Baba wangu; usisimame mbali nami, Baba wangu. 22Fanya haraka kunisaidia , Ee Baba wangu Mwenye Enzi, wokovu wangu.