Raba Yaanguka na Daudi Avaa Taji
20 1Wakati wa mwaka kupindukia, majira wafalme watokapo kwenda vitani, Yoabu aliuongoza jeshi likatoka, akaiharibu nchi ya Waamoni, kisha akaenda akauzingira mji wa Raba, huku Daudi akikaa Yerusalemu. Yoabu akaupiga Raba, akaubomoa. 2Daudi akaitwaa taji kutoka kichwani mwa mfalme wao. Ilikuwa na uzito wa pauni kama sabini na tano za dhahabu, na ilikuwa imepambwa kwa kito cha thamani, nayo ikawekwa juu ya kichwa cha Daudi. Pia akachukua nyara nyingi mno kutoka mjini. 3Akawatoa watu waliokuwamo ndani yake, akawaweka katika kazi ya misumeno, na sululu za chuma, na mashoka. Vivyo hivyo Daudi akaifanyia miji yote ya Waamoni. Kisha Daudi na jeshi lake lote wakarudi Yerusalemu.
Majitu Yaanguka kwa Mkono wa Israeli
4Baada ya haya, vita vikatokea na Wafilisti huko Gezeri. Wakati huo Sibekai Mhushathi akamwua Sipai, mmoja wa wazao wa Rafa, nao Wafilisti wakashindwa.
5Vita vikatokea tena na Wafilisti. Elhanani mwana wa Yairi akamwua Lahmi, ndugu yake Goliathi Mgiti, ambaye mpini wa mkuki wake ulikuwa mnene kama mti wa mfumaji. 6Mara nyingine tena vita vikatokea huko Gathi, mahali palipokuwa na mtu mkubwa mno, mwenye vidole sita katika kila mkono na vidole sita katika kila mguu, ishirini na vinne jumla—naye pia alizaliwa kwa Rafa. 7Alipoitukana Israeli, Yonathani mwana wa Shimea, ndugu yake Daudi, akampiga akamwua. 8Hawa walizaliwa kwa Rafa huko Gathi, nao wakaanguka kwa mkono wa Daudi na kwa mkono wa watumishi wake.