Esta Anasogea Katika Kiti cha Enzi cha Mfalme
5 1Siku ya tatu, Esta akavaa mavazi ya kifalme, akasimama katika ua wa ndani wa jumba la mfalme, akiuelekea ukumbi wa mfalme. Naye mfalme alikuwa ameketi juu ya kiti chake cha enzi ndani ya ukumbi, akiuelekea mlango wa jumba. 2Mfalme alipomwona Malkia Esta amesimama katika ua, akapata kibali mbele yake, naye akamnyooshea ile fimbo ya dhahabu iliyokuwa mkononi mwake. Basi Esta akasogea, akaugusa ncha yake.
3Mfalme akamwuliza, "Una nini, Malkia Esta? Ni ombi gani lako? Hata nusu ya ufalme utapewa."
4Esta akasema, "Kama ikimpendeza mfalme, na aje mfalme pamoja na Hamani leo kwenye karamu niliyoiandaa."
5Mfalme akasema, "Mleteni Hamani upesi ili tufanye kama Esta alivyosema." Basi mfalme na Hamani wakaja kwenye karamu aliyoiandaa Esta.
6Walipokuwa wakinywa divai, mfalme akamwuliza Esta, "Ni haja gani yako? Nawe utapewa. Nalo ombi lako ni nini? Hata nusu ya ufalme—ni yako."
7Esta akajibu, "Haja yangu na ombi langu ni hili: 8Kama nimepata kibali mbele ya mfalme, na kama ikimpendeza kunikubalia haja yangu na kunitimizia ombi langu, basi mfalme na aje pamoja na Hamani kwenye karamu nitakayowaandalia. Kesho nitafanya kama mfalme asemavyo."
Ghadhabu ya Hamani Yamgeukia Mordekai
9Siku ile Hamani akatoka akiwa na furaha na moyo mkunjufu. Lakini alipomwona Mordekai kwenye lango la mfalme, wala hakusimama wala kutetemeka mbele yake, Hamani akajaa ghadhabu juu ya Mordekai. 10Hata hivyo, Hamani akajizuia, akaenda nyumbani kwake. Akatuma watu wawaite rafiki zake na Zereshi mkewe, 11Hamani akawaeleza fahari ya utajiri wake, na wingi wa wanawe, na jinsi mfalme alivyomheshimu na kumpandisha cheo juu ya wakuu na watumishi wa mfalme.
12Hamani akaongeza, "Wala si hayo tu. Malkia Esta hakumwalika mtu mwingine pamoja na mfalme kwenye karamu yake ila mimi peke yangu, nami nimealikwa tena kesho pamoja na mfalme. 13Lakini haya yote hayanifai kitu kila ninapomwona Mordekai, yule Myahudi, ameketi kwenye lango la mfalme."
14Zereshi mkewe na rafiki zake wote wakamwambia, "Waamuru watengeneze mti wenye kimo cha dhiraa hamsini. Asubuhi mwombe mfalme atundikwe Mordekai juu yake. Ndipo uende pamoja na mfalme kwenye karamu ukiwa na furaha." Jambo hili likampendeza Hamani, akausimika ule mti.