Mfalme Amheshimu Mordekai
6 1Usiku ule, usingizi ukamkimbia mfalme; akaamuru kitabu cha kumbukumbu—yaani tarehe—kiletwe na kusomwa mbele yake. 2Ikaonekana imeandikwa kwamba Mordekai alikuwa amewashtaki Bigthana na Teresho, matowashi wawili wa mfalme waliolinda mlango, waliotafuta kumuua Mfalme Ahasuero. 3Mfalme akauliza, "Ni heshima gani na ukuu gani ambao Mordekai amepewa kwa jambo hili?" Watumishi wake wakajibu, "Hakufanyiwa lolote."
4"Ni nani aliye ukumbini?" mfalme akauliza. Hamani alikuwa ameingia ukumbi wa nje wa jumba la mfalme ili kumwomba amtundike Mordekai kwenye mti aliokuwa ameuandaa.
5Watumishi wa mfalme wakamwambia, "Tazama, Hamani amesimama ukumbini." "Mwingizeni ndani," mfalme akasema.
6Hamani akaingia. Mfalme akauliza, "Afanyiwe nini mtu ambaye mfalme apenda kumheshimu?" Hamani akawaza moyoni, "Ni nani ambaye mfalme angependa kumheshimu kuliko mimi?"
7Basi Hamani akamwambia mfalme, "Kwa mtu ambaye mfalme apenda kumheshimu, 8na waletwe vazi la kifalme ambalo mfalme amevaa, na farasi ambaye mfalme amepanda, na taji ya kifalme kwa ajili ya kichwa chake. 9Vazi hilo na farasi vikabidhiwe mmoja wa maafisa waheshimiwa wa mfalme. Wamvike yule mtu ambaye mfalme apenda kumheshimu, wampandishe juu ya farasi katika uwanja wa mji, na kutangaza mbele yake, 'Hivi ndivyo afanyiwavyo mtu ambaye mfalme apenda kumheshimu!'"
10"Haraka," mfalme akamwambia Hamani, "chukua vazi na farasi kama ulivyosema, umfanyie hivyo Mordekai Myahudi aketiye langoni pa mfalme. Usiache lolote katika yote uliyoyasema."
11Hamani akachukua vazi na farasi, akamvika Mordekai, akampandisha juu ya farasi katika uwanja wa mji, akitangaza mbele yake, "Hivi ndivyo afanyiwavyo mtu ambaye mfalme apenda kumheshimu."
12Baadaye Mordekai akarudi langoni pa mfalme, lakini Hamani akaharakisha kwenda nyumbani kwake, akiomboleza, na kichwa chake kimefunikwa. 13Hamani akamweleza Zereshi mkewe na rafiki zake wote kila kitu kilichokuwa kimetokea. Washauri wake na Zereshi mkewe wakamwambia, "Kwa kuwa Mordekai, ambaye umeanza kuanguka mbele yake, ni Myahudi, hutaweza kumshinda—hakika utaanguka mbele yake." 14Walipokuwa bado wakizungumza naye, matowashi wa mfalme wakafika, wakamhimiza Hamani aende haraka kwenye karamu ambayo Esta alikuwa ameiandaa.