Elihu Anena Tena
35 1Kisha Elihu akaendelea, akasema: 2"Je, wadhani hili ni haki? Wasema, 'Haki yangu ni kubwa kuliko ya Mungu.' 3Kwa maana wauliza, 'Yakufaa nini? Nafaidi nini nisipofanya dhambi?' 4Nitakujibu, wewe na rafiki zako pamoja nawe. 5Tazama juu mbinguni ukaone; angalia mawingu, yaliyo juu kuliko wewe. 6Kama ukifanya dhambi, watimiza nini juu yake? Na kama maasi yako ni mengi, wamtendea nini? 7Kama uki mwenye haki, wampa nini yeye? Au apokea nini mkononi mwako? 8Uovu wako wamwathiri mtu kama wewe tu, na haki yako yamhusu binadamu mwenzako tu. 9Watu walia kwa uzito wa dhuluma nyingi; waomba msaada dhidi ya mkono wa wenye nguvu. 10Lakini hakuna asemaye, 'Yuko wapi Mungu Muumba wangu, atoaye nyimbo wakati wa usiku, 11atufundishaye zaidi ya wanyama wa nchi na kutufanya kuwa na hekima kuliko ndege wa angani?' 12Hapo walia, lakini hatoi jibu, kwa sababu ya kiburi cha watu waovu. 13Hakika Mungu hasikilizi kilio kisicho na maana; Mwenyezi hakizingatii. 14Sembuse basi atakapojibu usemapo kwamba humwoni yeye—ingawa shauri lako liko mbele zake nawe lazima umngoje. 15Na sasa, kwa sababu hasira yake bado haijaadhibu, naye hakuzingatia sana upumbavu. 16Ayubu afungua kinywa chake kwa maneno matupu; azidisha maneno bila maarifa."