Elifazi Anena
4 1Ndipo Elifazi Mtemani akajibu: 2"Kama mtu akithubutu kusema neno nawe, je, utachoka? Lakini ni nani awezaye kujizuia asinene? 3Tazama, wewe umewafundisha wengi, nawe umeitia nguvu mikono iliyo dhaifu. 4Maneno yako yamemwinua yeye ajikwaaye, nawe umeyaimarisha magoti yaliyolegea. 5Lakini sasa limekujia wewe, nawe umechoka; limekugusa, nawe umefadhaika. 6Je, kumcha kwako Mungu si tumaini lako, na uadilifu wa njia zako si taraja lako? 7Kumbuka sasa: ni nani, aliye hana hatia, aliyepata kuangamia? Ni wapi wanyofu walipopata kuharibiwa? 8Kama nilivyoona mimi, wale walimao uovu na kupanda taabu huvuna vilevile. 9Kwa pumzi ya Mungu wao huangamia, na kwa mvumo wa hasira yake huteketea. 10Ngurumo ya simba, sauti ya simba mkali, meno ya wana-simba— yamevunjika. 11Simba hodari huangamia kwa kukosa mawindo, na wana wa simba jike hutawanyika. 12Basi neno lililetwa kwangu kwa siri; sikio langu likapata mnong'ono wake. 13Katikati ya mawazo yasumbuayo yatokanayo na maono ya usiku, hapo usingizi mzito uwaangukiapo watu, 14hofu ikanijia, na tetemeko, nayo ikaifanya mifupa yangu yote itetemeke. 15Roho ikapita mbele ya uso wangu; nywele za mwili wangu zikasimama wima. 16Ilisimama kimya, lakini sikuweza kuutambua umbo lake. Sura ilikuwa mbele ya macho yangu; kukawa kimya, kisha nikasikia sauti: 17'Je, mwanadamu aweza kuwa mwenye haki mbele za Mungu? Je, mtu aweza kuwa safi mbele za Muumba wake? a a v17 Elifazi anamchora Mungu kama hakimu aliye mbali ambaye mbele yake hakuna mwanadamu awezaye kusimama — ndio mtazamo ambao rafiki hao watatu hawatawahi kujinasua kutoka kwao, na ndio mtazamo ambao sura za mwisho za kitabu hiki zinaufunua kuwa ni kutomjua Baba yetu. 18Tazama, hawaamini watumishi wake, naye huwashtaki malaika zake kwa kosa; 19sembuse wale wakaao katika nyumba za udongo, ambao msingi wao uko mavumbini, wasiopondwapondwa kama nondo. 20Kati ya asubuhi na jioni huvunjwa vipande vipande; bila kutambuliwa, huangamia milele. 21Je, kamba ya hema yao haing'olewi ndani yao? Hufa bila kamwe kupata hekima.'" b b v21 Mfano wa kamba ya hema unaonyesha uhai kama hema: kamba iking'olewa, jengo lote huanguka na kutoweka.