Amri za Baba, Uzima wa Mwana
3 1Mwanangu, usisahau mafundisho yangu, bali moyo wako uzishike amri zangu, 2kwa maana zitakuongezea wingi wa siku na miaka ya uzima na amani. 3Upendo wa agano na uaminifu visikuache; vifunge shingoni mwako, viandike katika kibao cha moyo wako. 4Ndipo utapata kibali na sifa njema mbele za Baba yetu na mbele za watu.
5Mtumaini Baba yetu kwa moyo wako wote, wala usizitegemee akili zako mwenyewe. 6Katika njia zako zote mkiri yeye, naye atayanyoosha mapito yako.
7Usiwe na hekima machoni pako mwenyewe; mche Baba yetu, ukajiepushe na uovu. 8Jambo hili litauletea mwili wako uponyaji na mifupa yako uburudisho.
9Mheshimu Baba yetu kwa mali yako na kwa malimbuko ya mazao yako yote, a a v9 Malimbuko yalikuwa sehemu ya kwanza na iliyo bora ya mavuno, iliyotolewa kwa Baba yetu kabla ya sehemu yoyote kutumika. 10ndipo ghala zako zitajaa tele, na mapipa yako yatafurika divai mpya.
11Mwanangu, usidharau adhabu ya Baba yetu wala usichoke kwa maonyo yake, 12kwa maana Baba yetu humrudi yule ampendaye moyoni mwake, kama vile baba amrudivyo mwana apendezwaye naye.
13Heri mtu yule aonaye hekima, na mtu yule apataye ufahamu, 14kwa maana faida yake ni bora kuliko faida ya fedha, na mapato yake ni bora kuliko dhahabu. 15Yeye ni wa thamani kuliko marijani, na hakuna kitu unachokitamani kiwezacho kulinganishwa naye. 16Uzima wa siku nyingi u katika mkono wake wa kuume; katika mkono wake wa kushoto mna utajiri na heshima. 17Njia zake ni njia za kupendeza, na mapito yake yote ni amani. 18Yeye ni mti wa uzima kwa wale wamshikao; na wale wamshikiliao sana huitwa heri.
19Baba yetu kwa hekima aliiweka misingi ya nchi; kwa ufahamu aliziimarisha mbingu; 20kwa maarifa yake vilindi vilipasuka, na mawingu hudondosha umande.
21Mwanangu, usiviache haya vitoke machoni pako; shika hekima kamili na busara, 22navyo vitakuwa uzima wa nafsi yako na pambo la shingo yako. 23Ndipo utakwenda katika njia yako salama, na mguu wako hautajikwaa. 24Ulalapo, hutaogopa; naam, utakapolala, usingizi wako utakuwa mtamu. 25Usiogope hofu ya ghafula, wala uangamivu wa waovu utakapokuja, 26kwa maana Baba yetu atakuwa tumaini lako, naye atauhifadhi mguu wako usinaswe.
27Usiwanyime wema wale wanaostahili, wakati uwezapo kuutenda. 28Usimwambie jirani yako, "Nenda, urudi tena, na kesho nitakupa"—wakati unacho kitu hicho. 29Usimfanyie jirani yako hila ya uovu, aketiye kando yako kwa kukuamini. 30Usishindane na mtu bila sababu, ikiwa hakukutenda mabaya.
31Usimwonee wivu mtu mwenye jeuri, wala usichague njia yake yoyote, 32kwa maana mtu mpotovu ni chukizo kwa Baba yetu, bali wanyofu huwaweka katika siri yake. 33Laana ya Baba yetu i katika nyumba ya waovu, bali huibariki maskani ya wenye haki. 34Kwa wenye dhihaka yeye hudhihaki, bali wanyenyekevu huwapa neema. 35Wenye hekima watarithi heshima, bali wapumbavu hupata fedheha peke yake.