Asafu Alia Katika Giza
Kwa mwimbishaji; mtindo wa Yeduthuni. Zaburi ya Asafu.
Asafu hawezi kulala wala kusema, naye anauliza swali ambalo watu huogopa kuuliza: je, upendo wa Baba yake umekoma, je, amesahau kufanya neema? Hakuna kinachobadilika ila kumbukumbu yake. Kwa makusudi anaikumbuka bahari, mahali ambapo njia ilikuwa halisi na nyayo hazikuonekana.
77 1Napaza sauti yangu kwa Baba yetu; sauti yangu inamwendea Baba yetu, ili anisikie. 2Katika siku ya taabu yangu nalimtafuta Baba Mwenye Enzi; usiku mkono wangu ulinyoshwa wala haukuchoka; nafsi yangu ilikataa kufarijiwa. 3Namkumbuka Baba yetu, nami naugua; natafakari, na roho yangu inazimia. Sela.
4Uliyashika makope ya macho yangu yasifumbe; nalifadhaika nisiweze kunena. 5Naliziangalia siku za zamani, miaka ya nyakati za kale. 6Naliikumbuka nyimbo yangu wakati wa usiku; nalitafakari moyoni mwangu, na roho yangu ikauliza-uliza: 7"Je, Baba Mwenye Enzi atakataa milele, wala hataonyesha tena upendeleo? 8Je, upendo wake wa agano umekoma milele? Je, ahadi yake imefikia mwisho kwa vizazi vyote? 9Je, Baba yetu amesahau kuwa na neema? Je, kwa hasira amezuia huruma zake? Sela.
10Ndipo nikasema, "Hili ndilo ombi langu: miaka ya mkono wa kuume wa Aliye Juu." a a v10 Ombi hili ni kwa miaka iliyopita ambapo mkono wenye nguvu wa Aliye Juu ulitenda kwa uweza kwa ajili ya watu wake. 11Nitayakumbuka matendo ya Baba yetu; naam, nitayakumbuka maajabu yako ya zamani. 12Nitatafakari juu ya kazi yako yote, na kuyaangalia matendo yako makuu. 13Njia yako, Baba yetu, ni takatifu. Ni mungu yupi aliye mkuu kama Baba yetu? 14Wewe ndiwe Baba yetu utendaye maajabu; umedhihirisha nguvu zako kati ya mataifa. 15Kwa mkono wako uliwakomboa watu wako, wana wa Yakobo na Yusufu. Sela.
16Maji yalikuona, Baba yetu; maji yalikuona, yakajitaabisha; naam, vilindi vikatetemeka. 17Mawingu yalimwaga maji; anga zilinguruma kwa radi; mishale yako ikaruka pande zote. 18Sauti ya radi yako ilivuma katika kisulisuli; umeme wako uliangaza ulimwengu; nchi ikatetemeka na kutikisika. 19Njia yako ilikuwa baharini, mapito yako katika maji makuu; lakini nyayo zako hazikuonekana. 20Uliwaongoza watu wako kama kundi la kondoo kwa mkono wa Musa na Haruni.