Laiti Ningeweza Kumpata
23 1Ndipo Ayubu akajibu: 2"Hata leo malalamiko yangu ni machungu; mkono wake ni mzito juu ya kuugua kwangu. 3Laiti ningejua pa kumpata, ili nifike hata makao yake! 4Ningeweka mashtaka yangu mbele zake na kujaza kinywa changu hoja. 5Ningejifunza maneno ambayo angenijibu na kuelewa yale ambayo angeniambia. 6Je, angeshindana nami kwa ukuu wa nguvu zake? La—bila shaka angenisikiliza. 7Hapo mtu mnyofu angeweza kuhojiana naye, nami ningeachiliwa huru milele na mwamuzi wangu. 8Lakini niendapo mashariki, hayupo; nami magharibi siwezi kumpata. 9Afanyapo kazi kaskazini, siwezi kumwona; ageukapo kusini, siwezi kumpata. 10Lakini yeye anaijua njia niiendeayo; atakaponijaribu, nitatoka kama dhahabu. 11Mguu wangu umeshika nyayo zake; nimeishika njia yake wala sikugeuka kando. 12Sikuiacha amri ya midomo yake; nimeyathamini maneno ya kinywa chake kuliko chakula changu cha kila siku. 13Lakini yeye habadiliki—ni nani awezaye kumzuia? Chochote akitakacho, hukifanya. 14Kwa maana atatimiza yale aliyoniagizia, na mambo mengi kama hayo yamo moyoni mwake. 15Ndiyo sababu ninatetemeka mbele zake; niyafikiripo, ninamwogopa. 16Mungu ameufanya moyo wangu kuzimia; Mwenyezi amenitia hofu. 17Lakini sikunyamazishwa na giza, wala na kiza kinene kinifunikacho uso wangu."