Kwa Nini Mwenyezi Haweki Nyakati
24 1"Kwa nini Mwenyezi haweki nyakati za hukumu? Kwa nini wale wamjuao kamwe hawazioni siku zake? 2Waovu huhamisha mawe ya mpaka; hunyakua makundi na kuyachunga kama yao wenyewe. 3Humwondoa punda wa yatima; huchukua ng'ombe wa mjane kuwa rehani. 4Huwasukuma wahitaji watoke njiani, hata maskini wa nchi wanalazimika kujificha. 5Tazama—kama punda-mwitu jangwani, maskini hutoka kwenda kazini mwao, wakitafuta chakula; nyika huwapa watoto wao mkate. 6Huvuna malisho katika mashamba yasiyo yao na kuokota masalia ya shamba la mizabibu la mwovu. 7Hulala usiku uchi, bila nguo, bila cha kujifunika dhidi ya baridi. 8Hulowa kwa mvua za milimani na kujikusanya karibu na mwamba kwa kukosa hifadhi. 9Mtoto yatima hunyakuliwa kutoka kwenye titi, na mchanga wa maskini huchukuliwa kuwa rehani. 10Huzunguka uchi, bila nguo; wakiwa na njaa, hubeba miganda. 11Kati ya mibuni ya mizeituni hukamua mafuta; hufanya kazi ya mashinikizo ya divai, lakini wana kiu. 12Kutoka mjini wanaokufa hulia kwa uchungu, na koo za waliojeruhiwa hupiga kelele kuomba msaada—lakini Mungu hamshtaki yeyote kwa uovu.
13"Kuna wale wanaoiasi nuru; hawazijui njia zake wala kukaa katika mapito yake. 14Alfajiri muuaji huamka kuwaua maskini na wahitaji, na usiku huzurura kama mwizi. 15Jicho la mzinzi hungojea giza la jioni, akifikiri, 'Hakuna jicho litakaloniona,' naye huuficha uso wake. 16Gizani huvunja nyumba za watu; mchana hujifungia ndani, kwa maana hawataki kufanya lolote na nuru. 17Kwa maana giza nene ni asubuhi kwao wote; wamezoea vitisho vya giza.
18"Lakini wewe wasema wao ni wepesi juu ya uso wa maji; fungu lao la ardhi limelaaniwa, wala hakuna ageukiaye mashamba yao ya mizabibu. 19Kama vile ukame na joto huiondoa theluji iyeyukayo, ndivyo kaburi liwanyakuavyo waliotenda dhambi. 20Tumbo lililowazaa huwasahau; funza huwafanyia karamu; hawakumbukwi tena, na uovu huvunjwa kama mti. 21Humwinda mwanamke tasa asiyezaa mtoto na hawaonei mjane huruma.
22"Lakini kwa nguvu zake Mungu huwaburuta wenye nguvu; hujiinua, wala hakuna aliye na uhakika wa uhai wake mwenyewe. 23Mungu huwaacha wapumzike salama, nao hutegemea hilo, lakini macho yake yako juu ya njia zao. 24Hutukuzwa kwa kitambo kidogo, kisha hawapo tena; hushushwa chini na kukusanywa kama watu wote, hukatwa kama masuke ya nafaka. 25Kama si hivyo, ni nani awezaye kunithibitisha kuwa mwongo na kuyafanya maneno yangu kuwa si kitu?"