Vipimo Sahihi Ni Furaha Yake
11 1Mizani ya udanganyifu ni chukizo kwa Baba yetu, bali vipimo sahihi ni furaha yake. 2Kiburi kikija, ndipo huja aibu, bali hekima huja pamoja na wanyenyekevu. 3Uadilifu wa wanyoofu huwaongoza, bali ukaidi wa wadanganyifu huwaangamiza. 4Utajiri haufai kitu katika siku ya ghadhabu, bali haki huokoa na mauti. 5Haki ya wasio na hatia hunyoosha njia yao, bali mwovu huanguka kwa uovu wake mwenyewe. 6Haki ya wanyoofu huwaokoa, bali wadanganyifu hunaswa na tamaa yao wenyewe. 7Mtu mwovu afapo, tumaini lake hupotea, na matumaini yake katika nguvu zake mwenyewe huwa si kitu. 8Mwenye haki huokolewa na taabu, na mwovu huingia humo mahali pake. 9Kwa kinywa chake asiyemcha Mungu humwangamiza jirani yake, bali kwa maarifa wenye haki huokolewa. 10Mambo yaendapo vema kwa wenye haki, mji hufurahi, na waovu waangamiapo, huwa na vigelegele vya shangwe. 11Kwa baraka ya wanyoofu mji hutukuzwa, bali kwa kinywa cha waovu hubomolewa. 12Amdharauye jirani yake hana akili, bali mtu mwenye ufahamu hunyamaza kimya. 13Mchongezi huzunguka akifunua siri, bali mtu mwenye roho ya uaminifu huweza kuficha siri. 14Pasipo uongozi, watu huanguka, bali katika wingi wa washauri kuna usalama. 15Ajidhaminiye mgeni hakika atateseka kwa ajili yake, bali achukiaye kupeana mkono katika ahadi yu salama. 16Mwanamke mwenye neema hupata heshima, na watu wakatili hupata mali. 17Mtu mwenye fadhili hujinufaisha mwenyewe, bali mtu katili hujiletea taabu mwenyewe. 18Mwovu huchuma mshahara wa udanganyifu, bali apandaye haki huchuma thawabu ya kweli. 19Adumuye katika haki hupata uzima, bali afuatiaye uovu hukimbilia mauti yake mwenyewe. 20Wenye moyo mpotovu ni chukizo kwa Baba yetu, bali wale ambao njia zao hazina hatia ni furaha yake. 21Uwe na hakika mtu mwovu hataachwa bila adhabu, bali watoto wa wenye haki wataponyoka. 22Kama pete ya dhahabu katika pua ya nguruwe ndivyo alivyo mwanamke mzuri asiye na busara. 23Shauku ya wenye haki huishia katika mema tu, bali tumaini la waovu huishia katika ghadhabu. 24Mtu mmoja hutoa kwa ukarimu, lakini huzidi kutajirika; mwingine huzuia kilicho haki, na kuishia katika uhitaji. 25Nafsi ya ukarimu itaneemeshwa, na yeye awaburudishaye wengine naye mwenyewe ataburudishwa. 26Watu humlaani azuiaye nafaka, bali baraka huwa juu ya kichwa cha yeye aiuzaye. 27Autafutaye mema kwa bidii hutafuta upendeleo, bali autafutaye uovu, uovu utamjia. 28Autegemeaye utajiri wake ataanguka, bali wenye haki watastawi kama majani mabichi. 29Aletaye taabu juu ya nyumba yake mwenyewe atarithi upepo, na mpumbavu atakuwa mtumishi wa mwenye moyo wa hekima. 30Tunda la mwenye haki ni mti wa uzima, na avutaye roho za watu ni mwenye hekima. 31Ikiwa mwenye haki hulipwa duniani, je, si zaidi sana mwovu na mwenye dhambi!